Breaking News

UZAZI WA MPANGO UNAPUNGUZA VIFO VYA MAMA NA MTOTO

 Na Tonny Alphonce,Mwanza.

Wananchi wametakiwa kuendelea kutumia njia za uzazi wa mpango kwa kuwa matumizi ya njia hizo yanapunguza  vifo vya mama na mtoto kwa kiwango kikubwa.

Hayo yamesemwa jijini Mwanza na Dk Mathew Mourice Meneja Maria Stopes Mwanza wakati wa ufunguzi rasimi wa jengo la kutoa huduma za afya kwa kituo hicho  lililopo Gana wilayani Ilemela

Dk Mourice Amesema mama akizaa mfululizo bila kupumzika anaweza kudhoofika kiafya lakini kuongeza nafasi ya kifo upande wake au upande wa mtoto.

Dk Mourice amewataka wananchi waelewe kuhusu nia ya uzazi wa mpango ambayo haizuii idadi ya watoto wa kuzaa bali inasisitiza kuwepo kwa muda au nafasi kati ya mtoto mmoja na mwingine  ili kutoa nafasi kwa mama kuimarika kiafya kutoka ujauzito mmoja kwenda mwingine.

‘Tukiangalia mitaani kwa Mwanza kuna watoto wengi wa mtaani ambao wameshindwa kulelewa na familia kwa kukosekana kwa uzazi wa mpango na kama jamii itatumia njia za uzazi wa mpango  tunaweza kumaliza tatizo hili la watoto wa mtaani’.alisema Dk Mourice.

Ester Ibrahimu afisa wa masoko Marie Stopes amewataka wa kazi wa jiji la Mwanza kukitumia vema kituo hicho kipya kwa kuwa huduma zimeongezeka upande wa mama na mtoto lakini pia kimeongezwa kitengo cha mawasiliano kwaajili ya wateja watakao kuwa na maswali.

Aidha Ester amesema kituo sasa tayari kina madaktari bingwa wa wanawake na watoto ambao watawahudumia kwa ukaribu wanawake na watoto na hivyo kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika kutokana na matibabu sahihi kwenda kwa mgonjwa.


Lidya Mashauri mkazi wa Mkuyuni jijini Mwanza ameshukuru kwa huduma za bure zinazotolewa wiki hii  na shirika hilo hasa  upande wa magonjwa ya kina mama na watoto na kuwataka wanawake kujitokeza ili waweze kupima afya zao.

Amesema ni wazi kuwa kina mama mara nyingi ndio hupata changamoto za kiafya hasa kipindi cha uzazi hivyo ni vizuri kutumia wiki hii ya matibabu bure kufanya uchunguzi wa afya zao.

No comments