Breaking News

KAMATI YA MIPANGO MIJI YAIBUA MADUDU JIJI LA MWANZA.

Na Manga Msalaba
Mwanza.
MVUTANO mkali umeibuka katika Baraza la Halmashauri ya Jiji la Mwanza baina ya madiwani na watendaji wa Idara ya Mipango Miji kuhusu kiwanja namba 19 kitalu KK kilichopo Nyakato Temeke Mwanza na kuzua sintofahamu.

Mgogoro huo umesabaisha taarifa ya Kamati ya Mipango Miji chini ya Mweneyekiti wake Hamidu Selemani kutojadiliwa kutokana na mapungufu mengi ikiwemo kutotekelezwa kwa maagizo yaliyowataka watalaamu wa Idara ya Mipango Miji, kuwasilisha nyaraka muhimu za kiwanja hicho chenye mgogoro wa umiliki.

Mwenyekiti huyo amesema mapungufu hayo ni pamoja na kunyofolewa kwa maazimio ya kamati kuhusu vielelezo vya kiwanja 19 KK, vibali vya ujenzi wa vituo vya mafuta vinavyodaiwa kujengwa bila kufuata taratibu za kisheria.
Selemani aliayekuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa kamati yake Novemba 23 mwaka, alisema hata swali la papo kwa hapo lililoulizwa na Diwani wa Mabatini, Ntobi Boniphace pia halikuwemo kwenye taarifa aliyotakiwa kuwasilisha.

“Taarifa hii ina mapungufu mengi ikiwemo ya kiwanja namba 19 KK Nyakato Temeke kutoingizwa kwenye kabrasha hili lakini, kamati tuliazimia wataalamu wawasilishe barua inayotengua zuio la barua ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Mwanza, yenye Kumb.Na.LD/LZ/65837/22 aliyoandikiwa Mkurugenzi wa Jiji Agosti 31,2020 ikimtaka kusitisha hatua ya kukamilisha umiliki wa kiwanja hicho kwa Gain Company Ltd.

Alifafanua kuwa barua hiyo ilikuwa ikimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji hilo (wakati huo Kiomoni Kibamba), kusitisha ujenzi unaotekelezwa na kampuni hiyo kwenye kiwanja hicho.

Alieleza kuwa, kamati yake pia iliagiza muhtasari wa kikao cha kamati ya kugawa viwanja cha Agosti 30,2019 kilichothibitisha ombi la kampuni ya Gain kuomba kumilikishwa kiwanja hicho kilichopo eneo la viwanda lakini vyote vilikosekana kwenye kabrasha la taarifa ya kamati yake.

“Pamoja na mapungufu yake hayo mengi, naomba kuwasilisha taarifa hii ya robo ya kwanza ya mwaka wa 2021/2022 ambayo kama nisingeisaini kama anavyosema Mkurugenzi kuwa sikupaswa kuisaini kwa sababu ina mapungufu, isingeweza kuletwa kwenye baraza hili,” 

“Mengi ya msingi tuliyoazimia hayakuingizwa kwa makusudi ili kuficha nia mbaya iliyofanywa kwenye kiwanja hicho,” alisema Selemani.

Naye Diwani Ntobi alilieleza baraza hilo kuwa kamati hiyo imegundua uozo mwingi uliofanywa na wataalamu wa idara ya mipango miji na kuondoa baadhi ya vielelezo vya kiwanja hicho KK 19 na kingine namba 806 kilichopo Nyegezi.

Alieleza kuwa, wakati wa ziara yao ya Novemba 8 mwaka huu, wataalamu hao waliwadanganya na laiti mmiliki wa kiwanja hicho cha Nyagezi angekuwapo wangepata wakati mgumu na ama kushambuliwa na kujeruhiwa.

Awali wakati wa maswali ya papo kwa papo, Ntobi alichachamaa baada ya kuondolewa kwa swali lake, alilohoji kwenye kikao cha madiwani cha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhusu mgogoro wa umiliki wa kiwanja hicho na kumruhusu Gain kujenga bila kuwa na hati ya umiliki.

Diwani wa kata ya Nyamagana, Bhiku Kotecha, alisema katika kikao kilichopita wataalam waliiambia kamati hiyo kuwa sakata la kiwanja hicho KK 19, Msajili wa Hati alikataa kusaini rasimu ya hati ya umiliki wa Gain Company lakini baadaye walisema kiwanja hicho kina maelekezo ya viongozi wa juu serikalini.

“Yapo mambo mengi yanayopaswa kuchakatwa yaje kwa wajumbe maana tulipoomba barua inayotengua maelekezo ya Kamishna kuhusu kiwanja hicho na nyaraka nyingine za ujenzi wa vituo vya mafuta za miaka mitatu nyuma, walishindwa kuziwasilisha kwenye kamati hii,” alisema Kotecha.

Diwani huyo alishauri kuwa, kwa unyeti wa suala hilo na kwa maslahi mapana ya wananchi, hoja hiyo irudishwe tena kwenye Kamati ya Mipango Miji kabla ya kuletwa kujadiliwa kwenye baraza la madiwani lijalo.

Mkurugenzi wa Jiji hilo, Sekiete Yahaya, alikiri kuwa yaliyojadiliwa ndiyo kazi ya kamati ya Mipango Miji na kuongeza kwamba majibu yake yalipaswa kutolewe kwenye baraza hilo lakini kwakuwa jambo hilo lilikuwa halijaiva, aliafiki lirejeshwe kwenye kamati husika likachakatwe na kuletwa katika baraza lijalo.

Katika hatua nyingine Seleman aliliambia baraza hilo kuwa wajumbe wa kamati hiyo usalama wao uko hatari kutokana na kutishiwa maisha.

“Kuna maneno maneno huko nje, kuna nguvu kubwa na watu wenye akili nyingi kuhusu jambo hili lakini bahati nzuri kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya iko hapa, tunahitaji usalama wetu na ni haki yetu ya msingi mana tuko hapa kwa ajili ya maslahi ya wananchi,” alisema Selemani.

Kwa upande wake Naibu Meya wa Jiji, Rodrick Ngoye aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza hilo, alisema kutokana na unyeti ya jambo hilo baraza linaagiza wataalamu kukamilisha maagizo ya kamati, kuwasilisha vielelezo vinavyohitajika haraka na visichukue muda mrefu kwa sababu teknolojia ya mtandao imerahisha mawasiliano. 

Kwamujibu wa chanzo chetu cha habari kutoka ndani ya halmashauri hiyo, kiwanja KK 19 Nyakato chenye mita za mraba 3,000, kinamilikiwa na Seleman Karama lakini kiliuzwa zaidi ya sh. 400 ml kwa Gain Company Ltd ya Mwanza kwa madai kuwa umiliki wa Karama ulikuwa umefikia kikomo.

Imedaiwa kuwa, katika mauzo hayo serikali iliambulia sh 11 ml tu jambo ambalo limezua minong’ono mjini hapa kwani thamani ya kiwanja kama hicho kilicho eneo la viwanda, kingeuzwa kwa njia ya mnada serikali ingepata fedha nyingi zaidi. 

Karama ambaye alimilikishwa kiwanja hicho tangu mwaka 2008 analalamikia kubatilishwa kwa miliki yake kwa madai kuwa hajakiendeleza hivyo umiliki wake umeisha licha ya kukilipia kila mwaka na baadaye kuugua kwa muda mrefu na kupelekea kwenda nje ya nchi kwa matibabu.

“Nilibaini kuporwa kiwanja changu nilipokwenda kulipa kodi ya ardhi ya 2019/2020, baada ya kuomba Control number mhudumu aliyekuwepo aliniomba majina na namba ya kiwanja, alipoingiza majina na namba ya kiwanja alinieleza kuwa kiwanja hicho hakisomeki kwa majina yangu, ni mali ya Gain Company Ltd,” alieleza karama.

Mkurugenzi wa Gain Company Ltd aliyejitambulisha kwa jina moja la Peter, alisema kwa njia ya simu kuwa hawezi kutaja fedha alizonunua wala kuzungumzia suala hilo akidai ni la kipumbavu na kuongeza kuwa anachojua alikiomba na kuuziwa kihalali.

No comments