Breaking News

TAASISI ZAOMBWA KUWASILIANA ILI KUWA NA MGAWANYO MZURI WA MISAADA KWA WAHITAJI.

 Na Tonny Alphonce,Mwanza.

Taasisi na Mashirika yasiyo ya kiserikali yametakiwa kuwasiliana katika utendaji wao wa kazi ili misaada wanayoitoa iweze kwenda kwa walengwa wengi zaidi na kuepusha mlengwa mmoja kupatiwa msaada wa aina moja Zaida ya mara moja.

Kauli hiyo imetolewa na Mganga mfawidhi wa Zahanati ya Sawa ,Dr Herman Yohana wakati wakipokea msaada wa vitu mbalimbali kutoka Baraza la Watu Wanaishi na Virusi vya UKIMWI Tanzania (NACOPHA) tawi la Mwanza kwa niaba ya Kikundi cha Watoto wanaoishi na VVU cha Wisdom.

Dkt amesema kwa upande wa afya kuna mashirika mengi yanayotoa huduma hasa kwa watu wanaoishi na VVU na changamoto kubwa ni baadhi ya mashirika hayo kuwatafuta walengwa bila kuwasiliana na uongozi wa sehemu husika na kujikuta wanarudia kutoa msaada kwa familia ambazo tayari zimeisha saidiwa na mashirika mengine.

“Kwa mfano tuna familia nyingi zina Watoto ambao wamezaliwa na VVU sasa bila kuwa utaratibu mzuri baadhi ya familia zinajikuta hazijapata msaada wowote ndani yam waka mzima kwa sababu ya kukosekana kwa mawasiliano kati ya shirika moja na linguine”.alisema Dkt

Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo mwenyekiti wa kikundi cha Wisdom chenye Watoto wanaoishi na VVU kuanzia umri wa miaka 04 – 12 ,Sadu Yusuph amewashukuru NACOPHA kwa msaada waliowapatia ambao utawasaidia Watoto wenzao wanaondelea na masomo kwa hivi sasa.

Mwenyekiti wa kikundi cha Wisdom Sadu Yusuph akipokea msaada wa vitu mbalimbali kutoka kwa  Mratibu wa Mradi wa Hebu tuyajenge Bi Veronica Joseph kwa niaba ya kikundi cha watoto cha Wisdom.

Naye Mgdalena Mela ambae anamlea mtoto Salome Elias aliyezaliwa na VVU amelishukuru shirika la NACOPHA kwa msaada waliotoa na kuyataka mashirika mengine kuwasaidia Watoto wanaoishi na VVU kwa kuwa wengi wao wamepoteza wazazi wao na hivyo kuwa tegemezi.

Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa Hebu tuyajenge unaotekelezwa na NACOPHA,Bi Veronica Joseph amesema tayari kuna mazungumzo yanaendelea kuanzia ngazi ya mkoa ambapo mashirika yote yanayotoa huduma kwa watu wanaoishi na VVU watakutana na kupata njia nzuri ya kuwasiliana ili kuwafikia wahitaji kwa urahisi na kwa idadi kubwa.

Bi Veronica amesema NACOPHA inawajua watu karibia wote wanaoishi na VVU kwa kuwa mtandano wao umefika hadi ngazi ya familia hivyo mashirika yatakayohitaji mwongozo yameombwa kuwasiliana na NACOPHA.

Afisa maendeleo ya jamii mkoa wa Mwanza Bw Isack Ndasa amewashukuru watu binafsi na mashirika mbalimbali ambayo yamekuwa yakiyakumbuka makundi yenye uhitaji na kuyaomba kuhakikisha misaada wanayopata kutoka kwa wafadhili inatumika vile inavyotakiwa.

No comments