POMBE CHANZO CHA TATIZO LA AFYA YA AKILI KWA WATOTO.
Na Tonny Alphonce,Mwanza.
Wazazi wanao wanywesha pombe watoto wanapolia kwa muda
mrefu kwa lengo la kuwafanya walale wametakiwa kuacha tabia hiyo kwasababu
inachangia ongezeko la watoto wenye matatizo ya afya ya akili hapa nchini.
Wito huo umetolewa na Daktari bingwa na mbobezi wa watoto
na vijana ,Dkt Gema Sembele wakati akizungumzia sababu za matatizo ya afya ya
akili katika jamii na namna kujikinga na matatizo hayo.
Dkt Gema amesema mzazi anapompa pombe mtoto anamuweka
kwenye hatari ya kupata matatizo ya afya ya akili kwa kuwa katika kipindi cha
mwaka 0 – 5 hiki ni kipindi cha ukuaji wa ubongo wa mtoto hivyo kumnywesha
pombe mtoto katika umri huo kunaweza kuathiri ukuaji wa ubongo wa mtoto.
‘Kuna sababu nyingi zinazoweza kusababisha tatizo
la afya ya akili ikiwemo lishe duni wakati wa ujauzito wa mama,matumizi makubwa
ya pombe wakati mama anapokuwa mjamzito lakini pia tabia ya kuwanywesha pombe
Watoto wadogo ili waache kusumbua na kulala,hayo yote yanaweza kuwa sababu’alisema
Dkt Gema.
Kwa upande wake afisa lishe wa jiji la Mwanza, Joyce
Zelamala amesema lishe bora kwa mama mjamzito ni muhimu kwaajili ya maendeleo
ya mtoto na humsaidia mtoto kukua vizuri kimwili na kiakili.
Amesema kama mama mjamzito hatopata lishe bora kuna
uwezekano mkubwa kwa mama kupata madhara ya kiafya kama vile kutoongezeka
uzito,kupungukiwa damu na hata kujifungua mtoto mfu na kwa upande wa mtoto
lishe duni inaweza kusababisha ubongo kudumaa na mama kujifungua mtoto mwenye
tatizo la afya ya akili.
‘Mama ili ajifungue mtoto ambae yupo timamu
kimwili na kiakili lazima awe makini kipindi chote cha ujauzito wake,ale vizuri
aache kunywa pombe,kuvuta sigara au bangi na hata miadarati kwa sababu kipindi
cha ujauzito ni kipindi cha uumbaji kwa maana hiyo vitu vyote vya hatari mama
mjamzito lazima aviache’alisema Bi Zelamala.
Mwanasaikolojia Bwana Bosco Bosco amesema tatizo la
afya ya akili wakati mwingine husababishwa na sababu za kisaikolojia hasa kwa
watu wazima tofauti na watoto ambao wao sababu huwa ni za kibailojia zaidi.
Bw Bosco amesema watu wazima wengi wamepatwa na tatizo la afya ya akili kutokana na unywaji wa pombe kupitiliza,uvutaji wa vitu vya kulevywa kama Petroli,Mafuta ya taa,Gundi na matumizi ya dawa za kulevya kama heroin.
Amesema mtu akitumia vilevi hisia zake na mawazo yake yanavurugika
na hivyo kupelekea matatizo makubwa ya kitabia na kwa mtazamo wa nje mtu huyu
anaonekana hayupo sawa na amechanganyikiwa na kwa upande wa kiafya mtu huyu
tayari anakuwa na tatizo la afya ya akili.
Kauli mbiu ya Siku Ya Afya Ya Akili Duniani mwaka huu
inasema Afya ya akili katika Ulimwengu usio na usawa msisitizo ukiwa katika upatikanaji
wa huduma ya matatizo ya afya ya akili kutoka kwenye miji mikubwa na kushuka
chini hadi ngazi ya Zahanati ili kila mwananchi mwenye matatizo ya afya ya akili
apate matibabu.
No comments