Breaking News

 

NACOPHA YATIMIZA AHADI, YAKABIDHI CHELEANI KWA VIJANA WA PAZA SAUTI MWANZA.

Na Tonny Alphonce,Mwanza

Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (NACOPHA) kanda ya Mwanza wamekabidhi Cheleani ya kushona Mabegi kwa kikundi cha vijana cha Paza Sauti yenye thamani ya shilingi Milioni Moja na Nusu.



Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo meneja mradi wa Hebu Tuyajenge kanda ya Mwanza Bi Veronica Joseph amesema wameamua kuwapatia mashine hiyo baada vijana hao kuomba kupatiwa mashine hiyo wakati wa ziara ya Naibu katibu mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Uratibu na Bunge Ndg Kaspar Mmuya alipokitembelea kikundi hicho kwa nia ya kuona namna kikundi hicho kinavyofanya shughuli zake pamoja na utoaji elimu juu ya UKIMWI.



Bi Veronica amesema kupitia mashine hiyo ambayo inamota itawasaidia kuongeza uzalishaji wa mabegi  na vitu vingine wanavyotengeneza na hivyo kukuza uchumi kikundi na taifa kwa ujumla.

Akizungungumza kwa niaba ya wanakikundi wenzake mwenyekiti wa kikundi hicho cha Paza Sauti Angel Lurence amesema kwa muda mrefu walikuwa na uhitaji wa Cheleani yenye mota ambayo wamepatiwa hivyo sasa hivyo anamatumaini kuwa uzalishaji utaongezeka.



Angel amelishukuru Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (NACOPHA) kanda ya Mwanza kupitia mradi wa Hebu Tuyajenge kwa kuwapatia mashine hiyo na kuwataka kuendelea kuwasaidia kila watakapohitaji msaada wa kuhakikisha kikundi cha Paza Sauti kinakua na kuajiri vijana wengi zaidi wanaoishi na Virusi vya Ukimwi.



Kikundi cha Paza Suti ni kikundi cha Vijana wanaoishi na Virusi vya Ukimwi kilichopo Mwanza wilaya ya Nyamagana,kikundi hicho mbali ya kutoa elimu kwa vijana umuhimu wa kujikinga na UKIMWI lakini pia kikundi hicho kimekuwa kikifanya kampeni wa kuwarudisha watoro wa dawa za ARV kurudi kwenye matumizi sahihi ya ARV.

No comments