Serikali yaombwa kupanga bei elekezi kwa mazao yatokanayo na mifugo
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Umoja wa wajasiriamali wa ufugaji(UWAU) uliopo Mkoani Mwanza wameiomba Serikali kupanga bei elekezi kwa mazao yatokanayo na mifugo ili waweze kufuga kwa faida.
Akizungumza kwenye mafunzo ya siku moja yaliyoandaliwa na uongozi wa umoja huo yaliyolenga kutoa elimu ya ufugaji bora kwa wafugaji wa mifugo mbalimbali ikiwemo Kuku,Ng'ombe na Nguruwe Mwenyekiti wa wafugaji Kanda ya ziwa Rivinus Madarage alisema kuwa lengo lao ni kutaka kufuga ufugaji wenye tija katika Jamii.
Katibu tawala msaidizi ambe anasimamia uchumi na uzalishaji Mkoa wa Mwanza akizungumza na wajasiriamali wa ufugaji katika ukumbi wa Nyanza.
Madarage alisema kuwa Serikali iwasaidie kuzuia ama kulinda wajasiriamali wadogo wa ufugaji kwani malighafi za kutengeneza vyakula vya mifugo Kama vile mashudu ya pamba,mashudu ya alizeti,pumba za mahindi zinachukuliwa nje hali inayosababisha uhaba na mfumuko wa bei kwa bidhaa hizo, Jambo ambalo linaongeza gharama za uzalishaji na kusababisha kushindwa kujikwamua kiuchumi.
Aidha Madarage alieleza kuwa lengo Kuu la umoja wao Ni kuwawezesha wajasiriamali wa ufugaji Nchini kuelewa mbinu za ufugaji wenye tija utakaoleta manufaa kwa wanaumoja,jamii na Taifa kwa ujumla.
" Madhumuni ya umoja wetu Ni kuwaunganisha wajasiriamali wadogo wa ufugaji Kanda ya ziwa na kuwawezesha kupata elimu na mbinu mbalimbali katika ufugaji kwa kutumia fursa zilizopo Serikali I kuhusiana na mitaji, masoko na mnyororo wa thamani kwa mazao yatokanayo na ufugaji wenye tija",alisema Madarage
Kwaupande wa washiriki wa mafunzo hayo ambao pia ni wanaumoja wa UWAU walisema kuwa ufugaji unahitaji mtaji, muda lakini pia masoko hivyo ni vema Serikali ituwezeshe kuwa na bucha ya kuku yenye mashine za kisasa pamoja na majokofu.
Awali akizungumza katika mafunzo hayo kwaniaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Katibu tawala msaidizi anaesimamia uchumi na uzalishaji Emil Kasagara alisema kuwa Mkoa huu una viwanda viwili vya kusindika nyama vinavyomilikiwa na wawekezaji binafsi hivyo uwepo wa viwanda hivi ni fursa kwa soko la mifugo na mazao yake.
Alisema Mkoa unakiwanda kimoja cha kusindika maziwa ambacho kipo wilayani Sengerema na kinauwezo wa kusindika lita 500 kwa siku, pia upo mpango wa kuanzishwa kiwanda kikubwa Cha kusindika maziwa katika Wilaya ya Misungwi hivi karibuni, ambayo pia itakuwa fursa ya soko la maziwa yanayozalishwa katika Mkoa wa Mwanza.
Aidha, Kasagara aliwasihi kutumia minada kuuza mifugo yao kwani ndio sehemu maalum kwa ajili ya biashara ya Mifugo Kama Sheria ya nyama namba 10 ya mwaka 2006 inavyoeleza.
" Mkoa wa Mwanza unajumla ya minada 12 ya awali iliyopo chini ya usimamizi wa Halmashauri na mnada 1 wa upili(Nyamatala) ambao upo chini ya Wizara ya Mifugo na uvuvi ambapo biashara ya wanyama Kama Ng'ombe, Mbuzi na Kondoo hufanyika kwa siku tofauti tofauti",alisema Kasagara
Wajasiriamali wa ufugaji wakiwa kwenye mafunzo ya ufugaji bora.
No comments