Breaking News

Wekezeni nguvu katika kuongeza tija kwenye zao la pamba.



Na Hellen Mtereko, Mwanza

Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na wataalam wa kilimo Mkoani Mwanza wametakiwa kuwekeza nguvu  nyingi katika kuongeza tija kwenye zao la pamba ili kuwezesha Mkoa huo kuzalisha tani 70,000 za zao hilo huku kitaifa zikitarajiwa kuzalishwa tani milioni 1.

Hayo yamesemwa Jana na Barozi wa pamba Nchini,Aggrey Mwanri wakati akiwapatia mafunzo ya kuongeza tija kwenye uzalishaji wa zao la pamba  viongozi hao, ambapo alisema kampeni hiyo inalenga kuwapa ushauri utakaowafanya viongozi kuchukua uamuzi sahihi katika zao hilo.

Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na wataalam wa kilimo wakiwa kwenye mafunzo ya kampeni ya uzalishaji wa kuongeza tija katika zao la pamba


Alisema kuwa uzalishaji wa pamba kwa wakulima wetu ni kilo 100 hadi 300 kwa ekari, hauwezi kuwa na tija kwa sababu viwanda vinafungwa kwa kukosa malighafi  baada ya kufanya kazi kwa miezi minne na kwamba pamba thamani yake ya fedha haina tofauti na dhahabu au tanzanite zinatofautiana kwa matumizi.

Aliwataka viongozi hao wakawaelimishe wakulima vijijini wazingatie matumizi ya kanuni bora za kilimo, pembejeo bora,kipimo cha  cm 60x cm 30 kupanda mbegu kitakachowapa miche 44,444 badala ya kipimo cha cm 90 x cm 40 ambacho kimepitwa na wakati zaidi watumie mbolea zote  viwandani ya kupandia na kukuzia pamoja na samadi .

Awali Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel alisema Mkoa huo ni miongoni mwa Mikoa inayolima na kuzalisha zao la  pamba hivyo wakurugenzi wa kila Wilaya wahakikishe maofisa ugani wanakuwa na mashamba darasa ya mfano ya kuwafundishia  wakulima  ili wazalishe kilo 800 hadi 1000 kwa ekari.

Alisema mwaka 2016 /2017 uzalishaji wa pamba mkoani humu ulikuwa tani 11,531 ,mwaka 2017/18 zilizalishwa tani 17,376 huku mwaka 2018 /19 zikizalishwa tani 33,010 na 2019 /20 kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa zilipatikana tani 8,039.

Alisema pamba ni moja ya vyanzo vya mapato kwa wananchi , mavuno yalipofikia tani 33,010 yaliingiza sh. bilioni 39.612 hivyo tunaweza kuzalisha kwa tija kwa kuzingatia utaalam na wataalam hao watatuambia tuongeze  kitu gani na tukitembea pamoja tutafikia hata sh.bilioni  80 na  hiyo inawezekana .

Aggrey Mwanri Barozi wa zao la pamba Tanzania

Aliongeza kuwa ni wakati wa kujifunza kuzalisha kwa tija kwa kuzingatia wataalamu ambaye atasaidia kuelekeza nini kifanyike ili kuongeza uzalishaji .

" Tutahakikisha tunajipanga  na wataalamu ili elimu hiyo  ifike vijijini  ambako kuna wakulima ili kuwasaidia kutambua nini maana ya matumizi ya vipimo, mbolea,mbegu bora, viuadudu" Alieleza Gabriel.

Pia wakurugenzi wa halmashauri  watumie asilimia 10 ya ushuru  kuimarisha kilimo cha pamba na kihimiza maofisa  ugani vijijini kuanzisha mashamba darasa yaliyozingatia kanuni zote za kilimo bora yatumike kufundishia wakulima  ili kuongeza tija kwenye zao la pamba.


No comments