Breaking News

MKOA WA SINGIDA UNAFAHAMIKA KWA UZALISHAJI WA ALIZETI- MHE. MWENDA

 MKUU wa Wilaya ya Iramba Mhe.Suleiman Yusuph Mwenda amewataka Wananchi wa Mkoa wa Singida kutembelea Maonesho ya Wadau wa Alizeti yaliyoanza leo kwenye Uwanja wa Kanisa Katoliki Mkoa wa Singida.

Mhe.Suleiman amesema hayo leo alipotembelea Maonesho hayo ili kujionea namna ambavyo Maonesho hayo yatawasaidia Wakulima wa Zao la Alizeti wa Wilaya ya Iramba kuongeza uzalishaji na kupata masoko ya uhakika.

 “ Mkoa wa Singida unafahamika kwa uzalishaji wa Alizeti na nimetembelea Maonesho haya na nimejifunza mengi ambayo Wakulima wa Alizeti wanaweza kujifunza ambapo nimeona Wadau wanaozalisha pembejeo za kilimo kama mbegu, teknolojia za kilimo na Taasisi zinazotoa mikopo kwa Wakulima ” Alisema Mhe. Suleiman Yusuph Mwenda.

 Mhe. Mwenda amesema Wakulima ni Wadau muhimu katika mnyororo mzima thamani wa zao la Alizeti, hivyo ametoa rai kwa TanTrade kushirikiana na Wilaya yake kuandaa kuandaa Makongamano na Maonesho kama hayo ili kuwafikia Wakulima wengi zaidi.

 Kwa Upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) Bi.Latifa Khamis amesema Maonesho hayo yanaenda sambamba na Kongamano ambalo linalenga kuwakutanisha Wadau wote wa zao la Alizeti ili kujadili maendeleo ya sekta hiyo.

Pia kuna mafunzo yanayotolewa ili kuwajengea uwezo Wazalishaji wa zao la Alizeti kwa mujibu wa matakwa ya soko.

Ameongeza kuwa kutakuwa na Mikutano ya Biashara ya ana kwa ana (B2B) kwa njia ya mtandao ili kuwanganisha Wauzaji na Wanunuzi kutoka ndani na nje ya Nchi.

 “Hii sekta ni yakimkakati kwa Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na lengo ni kuongeza uzalishaji wa mafuta ya Alizeti na kupunguza uagizwaji wa mafuta yakupikia kutoka nje ya Nchi ” Alisema Bi. Latifa Khamis.

 Bi. Latifa ameeleza kuwa Mradi huu unatekelezwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kupitia Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) na Taasisi zingine kutoka Wizara mbalimbali chini wa ufadhili wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kupitia Jumuiya ya Nchi za Ulaya (EU).

 Kwa mujibu wa takwimu zilizopo sasa uzalishaji wa ndani unakidhi asilimia 43. Aidha nchi inazalisha tani 270,000 za mafuta ya kula kila mwaka na huagiza nyingine tani 600,000 kufidia pengo lililopo ndani.

Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mhe. Suleiman Yusuph Mwenda akiongea na Wadau wa  zao la Alizeti Mkoani Singida kwenye Kongamano la Wadau hao linalofanyika leo Mkoani Singida.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) Bi.Latifa Khamis (Aliyevaa ushungi) akiangalia taarifa za bidhaa za zao la Alizeti za mjasiliamali anayeshiriki kwenye Maonesho madogo ya Wadau wa  zao la Alizeti yanayofanyika sambamba na Kongamano la Wadau wa Alizeti leo Mkoa wa Singida.

Wadau wa Alizeti leo Mkoa wa Singida wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mhe. Suleiman Yusuph Mwenda.

No comments